Ajibu: Kwa chama hili, tunakosaje ubingwa

IBRAHIM Ajibu amekiangalia kikosi cha Simba kilichopo nchini Afrika Kusini na kisha akatikisa kichwa na kusema ‘kwa chama hili tunakosaje ubingwa.’

Mkali huyo wa asisti amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili kwenye dirisha hili kubwa la usajili akitokea Yanga ambayo iko kambini Morogoro. Simba kwa sasa ipo kambini Sauzi ambapo ilikwenda huko Jumatatu iliyopita na imekuwa ikifanya mazoezi kwenye Mji wa Rustenburg chini ya kocha Mbelgiji, Patrick Aussems.

Simba imefanya usajili kwa kuongeza nyota kadhaa wapya wakiwemo Gadiel Michael, Mkenya Francis Kahata, Deo Kanda (DR Congo), Wabrazili Tairone Santos da Silva, Gerson Fraga Vieira na Wilker Henrique da Silva.

Pia imemsaini Msudani, Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman, Beno Kakolanya, Kennedy Juma huku pia ikiwaongeza mikataba nyota wao wa msimu uliopita kama Meddie Kagere, Clatous Chota Chama, John Bocco, Shomary Kapombe, Pascal Wawa, Aishi Manula na wengineo.

Sasa Ajibu ameliambia Championi Jumamosi kuwa, kikosi chao ni kizuri na kinaundwa na wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu hivyo anaamini msimu ujao watafanya vizuri na hakutakuwa na sababu ya kushindwa kutwaa makombe.

“Simba iko vizuri kwa aina ya kikosi hicho ambacho kipo, hata ukiangalia wachezaji wake walivyo, kwa hiyo nina imani itafanya vizuri,” alisema Ajibu ambaye ana mke na mtoto mmoja.

Ajibu ambaye alikuwa nahodha wa Yanga msimu uliopita, ameongeza kwamba, hafahamu kama atapata namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo. “Sijajua kama nitapata namba kwenye timu, tuwe tu wavumilivu lakini pia watu wasubiri kuona nini ambacho nitakifanya katika klabu yangu hii,” aliongeza mchezaji huyo ambaye ana kidoti kwenye paji la uso

SWEETBERT LUKONGE NA SAID ALLY


Toa comment