Tanzania
This article was added by the user . TheWorldNews is not responsible for the content of the platform.

Nape; Tutumie mitandao ya kijamii kujiingizia kipato si kufanya umbea

Waziri wa Habari Mawasilino na Teknolojia, Nape Nnauye amewataka wananchi kutumia vizuri mitandao ya kijamii kwa kujiingizia kipato na kuacha kuitumia kwa mambo ambayo yanaweza kuvunja amani ya nchi na kuchafua utu wa mtu.

Aidha amesema pamoja na kuwa wanahakikisha wanalinda usalama wa jamii, ni muhimu pia kulinda utamaduni wa Bara la Afrika.

Nape ameyasema hayo leo Septemba 28, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mkutano wa Jukwaa la Uhuru wa Mitandao Barani Afrika uliohudhuliwa na wadau mbalimbali kutoka nchi tofauti.

Amesema wameweza kujadili changamoto, faida, fursa, wametoka wapi na wanaenda wapi katika dunia yote ya mitandao.

Amesema pamoja na nchi kutoa uhuru kwa wananchi, wanapaswa kulinda tamaduni kwa kutumia vizuri mitandao hiyo hasa kujiingizia kipato na si kutumia katika mambo ambayo yanaweza kuvunja amani ya nchi na kuchafua utu wa mtu.

“Tumeweka katika sera zetu uhuru wa mitandao lakini sasa hivi dunia imekua tutumie mitandao hii kufanya shughuli za kiuchumi na si kupiga umbea ambao haukusaidii chochote,”amesema Nape.

Amesema kuwa na uhuru mtandao unapaswa kuheshimiwa na kwamba  nchi za Afrika zinatakiwa kulinda tamaduni ili kuepusha nchi hizo kuingia kwenye matatizo ambayo yanasababisha kuharabika kwa amani au kuleta machafuko.

Aidha Nape amesema kuwa nchi inajipanga chaguzi zijazo ziweze kutumia teknolojia ili kumuwezesha kila mtu kuchagua viongozi popote atakapokua.

“Tunataka ifike mahali kila mwananchi awe na uwezo wa kupiga kura mtandaoni kusiwe na haja ya kwenda kwenye vituo na kupanga foleni, kama kila mtu anaweza kutumia simu basi inawezekana ni sisi kuamua kwa kuweka sera nzuri na utekelezaji,”ameongeza.

Amesema zaidi ya watu milioni 34 wapo kwenye mitandao na wanatumia Internet na wanaendelea kuweka mazingira mazuri ya sheria.

Naye Mbunge wa Viti Maalum, Neema lungangila amesema kuwepo kwa mkutano huo nchini kumetokana na juhudi zinazofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuifungua nchi kimataifa na kuimalisha uhuru wa habari,uhuru wa kujieleza na haki za binadamu.

“Bara Afrika wakati wa uchaguzi wamekuwa wakizima mitandao inazimwa wakati wa chaguzi zijazo mitandao isizimwe kwa sababu teknolojia imekua itafika mahali watu tutapiga kura mitandaoni,”amesema Lungangila.

Written by Janeth Jovin