Tanzania
This article was added by the user . TheWorldNews is not responsible for the content of the platform.

Rais Samia akitangaza Chuo cha Diplomasia sasa kuitwa Dk. Salim Ahmed Salim

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekitangaza Chuo cha Diplomasia kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam kuwa kuanza sasa kitaitwa jina la Dk. Salim Ahmed Salim “Center for Foreign Relations”.

Rais Samia ametangaza uamuzi huo jana Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa tovuti ya hifadhi ya nyaraka za Dk. Salim Ahmed Salim ambapo alisema hatua hiyo imetokana na mchango mkubwa wa kiongozi huyo katika kujenga uhusiano mzuri kati ya Tanzania na mataifa mengine.

Aidha Rais Samia alisema kuwa Dk. Salim ni Mtanzania mashuhuri ambaye alitoa mchango wake mkubwa katika kuliletea taifa la Tanzania maendeleo na Afrika kwa ujumla hivyo amesisitiza ni muhimu viongozi na watanzania kutambua mchango wa kiongozi huyo.

Alisema Dk. Salim katika nyanja ya kidiplomasia aliiwakilisha vyema Taifa la Tanzania katika nchi mbalimbali ikiwemo China, Umoja wa nchi huru Afrika, Marekani, Misri na India.

Naye Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alisema serikali imedhamiria kuja na mpango mkakati wa kuongeza bajeti itakayosaidia katika suala la kuhifadhi na kutunza kumbukumbu za viongozi mbalimbali wa Serikali kwa njia ya tovuti.

Alisema kuongezwa kwa bajeti hiyo ya kuhifadhi nyaraka kwa njia ya kidigitali itasaidia vijana na watanzania kwa ujumla kuweza kusoma na kujua historia ya nchi yao na bara la Afrika kwa ujumla kupitia Viongozi vyao.

Aidha Simbachawene alisema familia ya Dk. Salim umekuwa na mchango mkubwa katika kupatikana kwa taarifa za kiongozi huyo ambazo zitahifadhiwa kwenye tovuti maalum kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.