Tanzania
This article was added by the user . TheWorldNews is not responsible for the content of the platform.

Waziri Mavunde: Tanzania Iko Tayari Kushiriki Uchumi wa Madini Ya Bahari

*#Asema Tanzania imepokea fursa ya Bahari kwa mikono miwili*

Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa Tanzania iko tayari kushiriki uchumi wa Madini yaliyopo chini ya Sakafu ya Bahari Kuu ili kuongeza vyanzo vingine vya madini kwenye mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa na uchumi kwa ujumla.

Ameyasema hayo leo Oktoba 24, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akifunga Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Wakandarasi waliowekeza kwenye Madini yanayopatikana chini ya Sakafu ya Bahari Kuu.

Amesema kuwa Mkutano huo wa siku tatu ulioanza Oktoba 22 na kumalizika leo Oktoba 24, 2023 umesaidia taifa kuongeza fursa nyingine iliyopo katika uchumi wa madini na kwamba Tanzania itakuwa mshiriki mkubwa katika mnyororo mzima wa madini hayo.

“Wataalamu wa Serikali yetu kutoka Wizara na Taasisi zinazohusika na uchimbaji madini wamepata fursa ya kuwaongezea ujuzi wa shughuli za madini ya bahari kuu, hili linaonyesha imani ya ISA (Mamlaka ya Kimataifa ya Usimamizi wa Bahari Kuu) na Wakandarasi kwa Serikali yetu katika kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha utekelezaji mzuri wa Sehemu ya kumi na moja ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari (UNCLOS) na Mkataba wa 1994.” amesema Mhe. Mavunde.

Aidha, Mhe. Mavunde amesema kuwa Tanzania inasubiri kukamilika kwa Sheria ya Kimataifa itakayopelekea kuanza uvunaji wa madini hayo kwa kuzingatia athari za kimazingira kwa viumbe hai wanaopatikana chini ya Sakafu ya Bahari Kuu.

“Mkutano huo umeifungua macho Tanzania kuhusu uwepo wa fursa hiyo na tunaipokea kwa mikono miwili kwasababu ni wanachama wa ISA, sambamba na kuitangaza Sekta ya Madini ya Tanzania.” ameongeza Mhe. Mavunde

Pia, Waziri Mavunde ametumia fursa hiyo kuwakaribisha washiriki wa mkutano huo katika Mkutano wa Uwekezaji Katika Sekta ya Madini Tanzania chini ya kaulimbiu “Kufungua Uwezo wa Kuchimba Madini Tanzania kwa Baadaye” unaotarajiwa kufanyika kwa siku mbili, kuanzia tarehe 25 hadi 26 Oktoba, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Mamlaka ya Kimataifa ya Usimamizi wa Sakafu ya Bahari Kuu (ISA) Dkt. Marie Bourrel-MacKinnon amesema kuwa Tanzania itakuwa na mchango mkubwa katika uchumi utokanao na Madini yaliyopo chini ya Sakafu ya Bahari Kuu baada ya kukamilika kwa Sheria.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amesema kuwa kufanyika kwa mkutano huo hapa nchini umetokana na uongozi na kazi nzuri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kulifungua taifa na fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mathayo David ameeleza kuwa ni fahari kubwa kwa Tanzania kupewa nafasi ya kuandaa mkutano huo na kwamba utasaidia kutangaza fursa zilizopo katika Sekta ya Madini hapa nchini.