Tanzania
This article was added by the user . TheWorldNews is not responsible for the content of the platform.

NMB yawa benki ya tatu kwa faida Afrika Mashariki

Benki ya NMB imeshika nafasi ya tatu kwa ukubwa wa faida katika ukanda wa Afrika Mashariki, hii ni kutokana na mafanikio yake kiutendaji hasa ufanisi katika uendeshaji na utoaji wa huduma bora za kibenki nchini.

Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu benki hiyo imeweza kutengeneza faida baada ya kodi ya Shilingi Bilioni 262 ikiwa ni ongezeko la asilimia 27 ukilinganisha na nusu ya kwanza ya mwaka 2022.

Kutokana na kutengeneza kiasi hicho cha faida, NMB imeweza kushika nafasi ya tatu kwa ukubwa wa faida kati ya mabenki yote ndani ya ukanda huu wa Afrika Mashariki, ikitanguliwa na Benki ya Equity pamoja na Benki ya KCB zote kutoka nchini Kenya ambazo zimepata faida ya TZS bilioni 430 na TZS bilion 264 mtawalia. NMB imepanda kutoka nafasi ya 10 mwaka 2018 hadi kufikia nafasi ya tatu sasa.

Takwimu na uchambuzi wa hivi karibuni wa masoko ya hisa katika ukanda huu unaonyesha kuwa taasisi hiyo kubwa ya fedha nchini yenye mali zenye thamani ya zaidi ya Tsh Trilioni 11 imekua sana kiushindani na kuimarika sokoni katika miaka ya hivi karibuni, huku bei ya hisa zake sokoni ikiongezeka kwa takribani asilimia 28% tangu kutangazwa kwa matokeo yake ya kifedha ya nusu mwaka 2023 hadi kufikia shilingi 4,440 kwa kila hisa Septemba 8 2023.

Kutokana na kufanya vizuri kifedha, mtaji wa Benki ya NMB katika soko la hisa umekua kutoka Tsh 1.38 trilioni mwaka 2018 hadi kufikia mtaji wa kiasi cha Tsh 2.22 trillion Tarehe 8 Septemba 2023, hivyo kuifanya NMB kuwa kampuni ya pili kwa ukubwa katika soko la Tanzania ikitanguliwa na kampuni ya TBL na pia kampuni ya sita kwa ukubwa ndani ya kanda ya Afrika Mashariki, Shelisheli na Mauritus, ikitokea nafasi ya 14 mwaka 2019. Kampuni ya Safaricom Kenya ndiyo inayo ongoza katika ukanda huu ikiwa na mtaji wa zaidi ya shilingi trilioni nne.

Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi Ruth Zaipuna, mafanikio haya makubwa yanatokana na mazingira wezeshi ya kibiashara yanayowekwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na uimara wa uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Bi. Ruth aliongeza kuwa ufanisi wa taasisi hiyo pia umechangiwa na miaka mingi ya ukuaji endelevu pamoja na utekelezaji makini wa mpango mkakati wa uendeshaji wa benki hiyo.

Mwaka 2022, NMB ilipata faida kabla ya kodi ya shilingi bilioni 617 na kuweka historia ya faida kubwa kuwahi kutengenezwa na taasisi yoyote ya fedha nchini. Jarida la Euromoney limeitangaza benki ya NMB kama benki bora Zaidi Tanzania 2023, hii ikiwa ni mara ya 10 ndani ya miaka 11 kwa benki hiyo kubwa kupata tuzo hiyo inayo heshimika duniani kote.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Dkt. Edwin Mhede, alisema wamejipanga kuendelea kuchangia kikamilifu ukuaji wa uchumi wa nchi na ujenzi wa taifa kwa ujumla.