Tanzania
This article was added by the user . TheWorldNews is not responsible for the content of the platform.

Rais Samia: Watu Milioni 283 Afrika wanalala njaa kila siku

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa watu milioni 283 barani Afrika wanalala njaa kila siku, hali ambayo inachangia ongezeko la utapiamlo na magonjwa yanayotokana na lishe.

Rais Samia ameyasema hayo jana wakati akizungumza mbele ya washiriki wa Jukwaa la Mifumo ya Kilimo (AGRF), lililofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 5 hadi 8 mwaka huu.

Amesema Bara la Afrika lina ardhi nzuri yenye rutuba ila katika hali ya kushangaza watu wake milioni 283 wanalala njaa kila siku jambo ambalo ni la aibu na halikubaliki.

Rais Samia amewataka washiriki wa Jukwaa la AGRF, kutoka na maazimio ya namna gani nchi za Afrika zitaimarisha mifumo yake ya chakula.

Amesema changamoto zinazoikumba dunia nyakati hizi zinawafanya vijana wa Afrika kutaka mabadiliko ya sera katika sekta ya kilimo katika nchi zao ili kuwafanya wawekeze kwa ufanisi na tija.

“Afrika tumebaki kuwa walalamikaji badala ya kutoa suluhisho kutokana na utajiri wa rasilimali tulio nao, asilimia 65 ya ardhi yote inayofaa kwa kilimo ipo Afrika, tuna maji katika mito na maziwa makuu,” amesema Rais Samia

Amesema viongozi wa Afrika wanapaswa kufanya tathmini ya vipaumbele vyao kulingana na mahitaji yaliyopo ili kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo na kuwa na Afrika wanayoitaka.

Rais Samia amesema Afrika imejaliwa kuwa madini mengi hivyo uwekezaji katika sekta nyingine ikiwemo kilimo. Pia amebainisha mikakati mbalimbali ambayo Tanzania inaitekeleza katika sekta ya kilimo ikiwemo kuongeza bajeti ya kilimo.

Amesema kuanzia mwaka 2021/22 na 2023/24 bajeti ya kilimo iliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 125 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 400.

Rais Samia amesema Tanzania imedhamiria kuifanya sekta ya kilimo kuchangia asilimia 10 katika Pato la Taifa ifikapo mwaka 2030 kutoka asilimia nne ya sasa, kuyafikia masoko ya chakula ya kikanda ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Kiongozi huyo amesema serikali inaimarisha miundombinu kwa ajili ya kilimo biashara ikiwemo miundombinu ya usafirshaji na nishati ili kuharakisha na kurahisisha biashara na nchi zingine,”amesema Rais Samia

Amesema katika kuonesha dhamira hiyo inafikiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezielekeza benki za biashara kupunguza riba ya mikopo ya kilimo hadi kufikia asilimia tisa.

Aidha amesema programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) waliyoianzisha inalenga kuvutia vijana wengi kwenye kilimo biashara na mwitikio umeonesha matokeo chanya

Written by Janeth Jovin